|
SISI ni Watanzania wapigakura, wakazi wa jimbo la Njombe Kaskazini. Tunaandika kutoa maoni yetu huku mioyo yetu ikiwa ni mizito kwa uchungu usiomithilika. Kwanza tunaeleza kusikitishwa na namna zoezi zima la kura ya maoni kumsaka mgombea wa nafasi ya Ubunge toka ndani ya CCM lilivyoendeshwa jimboni kwetu.
Kulikuwa na wagombea 11, akiwamo mbunge aliyemaliza muda wake, Jackson Makweta. Hatuna maneno na wagombea wengine kumi ila mmoja wao tu.
Mgombea huyo pa,oja na kuwa na wadhifa mkubwa ndani ya CCM ngazi ya mkoa, hakuwa na sifa za kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge. Ni mgombea mwenye kasoro na upungugu mwingi kiasi ambacho angalazimisha vikao vya uteuzi ndani ya CCM kuliengua jina lake bila hata ya kuwa na majadiliano marefu.
Moja ya kasoro kubwa alizonazo ni elimu. Ana elimu ndogo ya darasa la pili. Kwa kiwango hicho cha elimu hawezi kuwa na upeo mpana wa kupambanua mambo, hasa aktika karne hii ya 21 ambayo ni ya sayansi na teknolojia.
Tanzania imeingia kwenye Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki, mbunge mwenye elimu ndogo ya darasa la pili ataweza kweli kupambana na changamoto zilizoko kwenye jumuiya hiyo? Kwa kutambia kwamba hana sifa, uwezo wala vigezo vya kuwa mbunge, aliamua kufanya kampeni zake kwa kutumia jina la Raos Jakaya Kikwete.
Katika kampeni zake, kwenye kura za maoni, alidai kwamba ametumwa na Rais kuja kugombea ubunge Njombe Kaskazini kwa lengo mahsusi la kumng’oa mbunge aliyemaliza muda wake, Jackson Makwetta.
Ili kuipa nguvu hoja ya kwamba alitumwa na rais kugombea ubunge njombe Kaskazini, alidai yeye ndiye aliyemshauri rais kuunda mkoa mpya wa Njombe na wilaya mpya ya Wanging’ombe. Alidai bila ya ushawishi na ukaribu wake kwa Rais, Mkoa na Wilaya mpya vingekuwa ndoto. Hatuamini kama rais anaweza kumshawishi na kumuunga mkono kugombea ubunge mtu mwenye elimu duni ya darasa la pili. Kampeni za mgombea huyo ‘ngumbaro’ kujinadi kuwa alitumwa na rais zilimbeba kwa kiwango kikubwa.
Sisi wapigakura wenye uelewa tunaona kuwa CCM imeamua kutudhalilisha wazi wazi kwa kutuletea mgombea ubunge mwenye elimu duni. Hii ni fedheha, tena ni aibu kubwa.
Tunadhani na kuamini udodoki aliokuwa akiuzungumzia hayati Baba wa Taifa Mwalimu nNyerere, ndani ya CCM umeshawadia. Hivyo sasa ni vyema sisi wananchi wa Njombe Kaskazini tukaiadibisha CCM kwa kutuchagulia mgombea wao. Tunasema jimbo la Njombe Kaskazini lipo wazi, tunawakaribisha wagombea kutoka vyama vingine. Tukithubutu kumchagua mgombea huyu wa CCM, tutachekwa leo hadi milele. Wali na pilau ni vya kupita, mbunge mbovu huacha makovu ya kudumu. Ni sisi wapigakura, Njombe Kaskazini.
|