
| Takukuru chunguzeni waliotokomea na fomu za kugombea | Send to a friend |
| Monday, 30 August 2010 22:50 |
|
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinasherehekea kile kinachodai baadhi ya wagombea wake wa ubunge na wa udiwani "kupita bila kupingwa" na hivyo tayari kujihakikishia ubunge na udiwani bila kulazimika kupigiwa kura na kushinda, katika uchaguzi mkuu uliotarajiwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu. Mpaka sasa wagombea karibu 20 wa ubunge kupitia CCM wametangazwa kupita bila kupingwa na hivyo tayari ni wabunge wateule katika majimbo yao na wanasubiri kuapishwa tu hapo mapema mwakani. Hata hivyo, mazingira yaliyowapatia wagombea wa CCM ushindi wa chee yanazusha maswali mengi bila majibu. Kwa mfano, tunaambiwa baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani walioteuliwa kugombea ubunge, katika mazingira ya kutatanisha, walipotea ghafla na kukata mawasiliano na vyama vyao muda mfupi tu baada ya kuchukua fomu za uteuzi na kuonekana baada ya siku ya uteuzi, hivyo kushindwa kurejesha fomu hizo na kuwafanya wagombea wa CCM kupita bila kupingwa. Wagombea wengine wa upinzani walitangaza kujitoa katika kinyang'anyiro cha ubunge muda mfupi tu baada ya kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) bila kutoa sababu za msingi, na hivyo kuwafanya wagombea wa CCM kupita bila kupingwa. Katika hali kama hii, tunalazimika kuhoji kama kweli wagombea wa CCM hawakupingwa, inavyooneka walipingwa, vyama vya upinzani viliteua watu wa kupambana na wagombea wa CCM, lakini kuna mchezo umechezwa nyuma ya pazia na ama wagombea wa CCM, au CCM yenyewe, kuhakikisha wagombea wa upinzani hawaendelei kugombea, na hivyo kuwawezesha wale wa CCM kupita bila kupinwa. Binafsi sitaki kuamini na nina imani wapo watanzania wengi ambao hawaamini kwamba watu hawa (wagombea wa upinzani) walichukua maamuzi hayo bila ushawishi wa mtu yeyote, kuna kila sababu ya kuamini kuwa watu hawa walishawishiwa kwa malipo maalum, kwa maneno mengine walipewa rushwa. Kama mtu ameomba katika chama chake nafasi ya kugombea ubunge na akapatiwa, halafu baadaye anachukua fomu ya uteuzi na kutokomea nayo mahala pasipojulikana na kuonekana baada ya siku ya uteuzi bila kusema kilichomsibu, kwanini tusiamini kuwa alichukua rushwa kutoka kwa mgombea wa CCM au CCM yenyewe ambao wamenufaika na mchezo huo mchafu? Kama hakuna rushwa iliyotembea kwa watu hawa na kwamba walibadili mawazo na kuamua kutogombea tena kama wanavyojaribu kujitetea, kwanini basi hawakuwasiliana na vyama vyao, ili vitafute wagombea wengine? Kwanini walikwenda mafichoni mpaka baada ya kupita kwa muda wa uteuzi? Ni nani anayeweza kuamini upuuzi huu? Wengine wamejitoa siku moja tu baada ya kuteuliwa na bila shaka wapo wengi watakaojitoa kadiri siku zinavyokwenda mbele, baadhi wakidai wamekosa kuwezeshwa kifedha na vyama vyao, na wengine wakitoa sababu zisizo na kichwa wala miguu, hali inayozidisha shaka ya watanzania wengi kuwa kuna mchezo mchafu unaoendelea wakati huu wa kampeni, kuhakikisha wagombea wengi wa CCM wanatangazwa kuchaguliwa bila kupingwa. Tuna kila sababu ya kuwatuhumu wagombea wa CCM na CCM yenyewe kuwa wanawanunua wagombea wa upinzani ili wajitoe, kutokana na ukweli usiopingika kuwa makao makuu ya rushwa yapo CCM, wagombea wengi wa CCM wamepata nafasi hizo kwa rushwa ndani ya chama chao, je, watashindwa kutumia rushwa nje ya chama ili kujipatia ubunge wa chee? Chama ambacho wanachama na viongozi wake wanahujumiana wao kwa wao, wenye hela wanawanunua wanachama na viongozi ili wapate uongozi, wanashindwa kweli kuwanunua wanachama wa vyama vya upinzani wanaogombea ubunge au udiwani ambao wengi wao ni njaa-kali? Pius Msekwa, makamu wa mwenyekiti wa CCM kitaifa kwa upande wa Tanzania bara, anapinga tuhuma za rushwa dhidi ya wagombea wa CCM kwa kutoa utetezi wa kipuuzi kabisa kwamba eti haiwezekani kuwahonga wapinzani kwasababu eti ni watu wazima! Hivi tangu lini rushwa ikatolewa kwa mtoto? Rushwa siku zote hutolewa kwa watu wazima tena wenye akili timamu na hadhi kubwa kwa jamii. Natoa changamoto kwa vyombo vya dola vinavyohusika na kupambana na kuzuia rushwa nchini, hususan TAKUKURU, kuwachunguza kikamilifu na kwa umakini wa hali ya juu, wanachama wa vyama vya upinzani waliotokomea na fomu na kusababisha wagombea wa CCM kupita bila kupingwa, pamoja na wale wanaojitoa kugombea baada ya kuteuliwa. TAKUKURU wanaweza kupata taarifa nzuri za kuwawezesha kufanya uchunguzi wao kutoka vyama ambavyo wanachama wake wanahusika na mchezo huu, na hata kwa kuwahoji wagombea wa CCM na viongozi wa chama hicho, nina hakika watapata ushahidi wa kuwawezesha kuwashitaki wahusika kwa vitendo vya rushwa kama kweli viongozi na wafanyakazi wa TAKUKURU wana dhamira ya kupambana na kuzuia rushwa nchini. |













