MwanzoContactsEmail
Home Uchambuzi Maoni ya Mhariri Serikali imeshindwa kudhibiti majanga ya moto?
BOOKMARK THIS PAGE
Serikali imeshindwa kudhibiti majanga ya moto?  Send to a friend
Monday, 30 August 2010 22:46

Tumesikitishwa na habari kwamba jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma limeteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana. Habari hizo zinasema kwamba moto huo ulioanza saa nne za usiku uliteketeza jengo zima, huku askari wa Kikosi cha Zimamoto, polisi na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiwa wameduwaa, wasijue la kufanya.

 Kuduwaa kwa viongozi hao wa mkoa kunatokana na ukweli kwamba mamia ya wafanyakazi wa ofisi hiyo, akiwemo mkuu wa mkoa mwenyewe, siyo tu kwamba hawana sehemu ya kufanyia kazi kuanzia jana, bali pia hawana nyaraka wala kumbukumbu zozote za kuwasaidia kufanya kazi zao. Baya zaidi ni hisia au dhana iliyoanza kujengeka miongoni mwa wananchi kwamba tukio hilo pengine limesababishwa na hujuma.

 Hivyo, pamoja na kwamba Mkuu wa Mkoa ameunda tume ya kuchunguza chanzo cha moto huo na kuorodhesha vitu vilivyoteketea katika jengo hilo, changamoto kubwa inayowakabili wafanyakazi wa ofisi hiyo hivi sasa ni jinsi ya kuendelea kufanya kazi pamoja huku wakilazimika kutawanyika katika ofisi mbalimbali zitakazowasetiri kwa muda. Hapana shaka kwamba suluhisho la muda la tatizo hilo litapatikana kwa gharama kubwa na itailazimu Serikali Kuu kuingilia kati haraka.

 Hata hivyo, ni bahati mbaya sana kwamba mpaka tunakwenda mitamboni changamoto hizo zilikuwa bado hazijaanza kufanyiwa kazi vilivyo, mbali na juhudi za viongozi wa mkoa huo kuhangaika kutafuta mchawi. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Msekela na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Stephen Zelothe, walikitupia lawama Kikosi cha Zimamoto ambacho, magari yake yaliishiwa maji na kushindwa kuuzima moto huo ambao umesababisha hasara kubwa.

Wakati tukiviachia vyombo na mamlaka husika kuzikabili changamoto hizo, tungependa kuishauri Serikali na kuiasa kwamba wakati sasa umefika wa kubuni mikakati endelevu ya kupambana na majanga ya moto katika nchi yetu. Kwa hali ilivyo hivi sasa, tunaweza kusema kwamba majanga hayo sasa yamekuwa matukio ya kawaida na ahadi za viongozi kuyamaliza zimekuwa zikichukuliwa na wananchi kama ngonjera zisizokwisha, kwani Serikali imeonyesha wazi kwamba haina ujasiri wa  kupambana na majanga hayo ya moto kwa vitendo.

Kwa muda mrefu sasa, sote tumekuwa mashuhuda wa majanga ya moto katika pembe zote za nchi yetu. Tumeshuhudia majanga hayo yakiteketeza mabweni na kutwaa maisha ya watoto wetu katika shule kadhaa, mbali na majanga hayo pia kuteketeza maisha ya watu, makazi na mali zao. Kwa udhaifu wetu, tumeacha vilio na simanzi vizame na kutawala nyoyo zetu, huku tukiwa wavivu wa kudai uchunguzi wa kina na hatimaye fidia stahiki.

Sisi tunapendekeza Serikali ichukue hatua zifuatazo: Kwanza, ihakikishe kwamba mifumo ya umeme katika majengo yake inafanyiwa mapitio, kwani majengo yake mengi yamekuwepo kwa zaidi ya miongo minne bila kukarabatiwa. Hii ni pamoja na kufunga vifaa vya kinga ya moto, vikiwemo vya kuhisi moshi na kuzima moto. Pili, Kikosi cha Zimamoto kiimarishwe kwa kupewa mafunzo na vifaa vya kisasa, na kukijenga upya kitengo cha ukaguzi wa nyumba za Serikali.
    
 Tatu, Kitengo cha Maafa kilichopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu siyo tu kipewe vifaa, bali pia kipandishwe hadhi kama taasisi inayojitegemea ili kiondokane na urasimu usiokuwa wa lazima. Nne, Serikali iingie katika mikataba na makampuni ya kufanya usafi siyo tu kwa sababu ya kuhakikisha majengo yake yanakuwa safi muda wote, bali pia kupunguza matumizi yatokanayo na ajira za kudumu za  wafanyakazi hao.

Ni imani yetu kwamba baada ya jengo lake kuteketea kwa moto, Serikali sasa itaona umuhimu wa kupambana na janga hilo kwa nguvu zote.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner