MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Habari Kikwet atoa ahadi mpya 15
BOOKMARK THIS PAGE
Kikwet atoa ahadi mpya 15  Send to a friend
Saturday, 28 August 2010 20:49


Leon Bahati
SIKU tisa baada ya kuanza kampeni mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete, ametoa ahadi kubwa 15 kwa wananchi wa mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa na Magharibi atakazotekeleza akipewa ridhaa ya kuongoza nchi kipindi kingine miaka mitano ijayo.
Baada ya kuzindua kampeni zake jijini Dar es Salaam Agosti 21, Kikwete aliendelea na kampeni zake katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Kigoma na leo anatarajia kuingia Rukwa kabla ya kwenda mkoani Mbeya.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika mikoa hiyo mitatu, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa taifa wa CCM, alisema akichaguliwa tena anakusudia kuweka rekodi ambayo Watanzania watamkumbuka kwa mazuri.
“Nawaahidi mambo mazuri zaidi katika miaka mitano ijayo kwa kuwaachia nchi iliyo nzuri zaidi, kwani nataka Watanzania wanikumbuke kwa mema. Sitaki nikumbukwe kwa lolote jingine,” alisema Rais Kiwete alipokuwa mkoani Mwanza.
Alisema amani ya nchi ni moja ya silaha zake kuu, hivyo akawahakikishia Watanzania kwamba, wakimchagua, atasimamia kikamilifu nchi kuepuka mizozo ya kidini, kikabila na kisiasa.
Rais Kikwete alisema katika kipindi hicho serikali yake pia italinda na kutetea Muungano na kuiboresha zaidi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ndani ya miaka mitatu.

Rais Kikwete alijibu malalamiko ya wananchi kwamba serikali imeshindwa kutelekeza adabu ya kungwa waliohukumiwa kifo kwa kuua albino akisema, hukumu hazijafikishwa mezani kwake ili atie sahihi kwa mujibu wa sheria utekelezaji wake ufanyike.

Hata hivyo,  aliahidi kuwa hukumu hizo zitakapofika mezani kwake atafanya uamuzi kama wanyongwe au la.

Kikwete alikiri kwamba kama ilivyokuwa serikali ya awamu ya tatu, hajawahi kutia saini kwa walihukumiwa kunyongwa, ili hukumu hiyo itekelezwe.

Akiwa mkoani Kagera, Rais Kikwete alitoa ahadi nyingi, lakini kubwa ni pamoja na kuwaahidi wanakijiji wa Misenyi wilayani Misenyi kwamba hawataondolewa katika eneo hilo ambalo awali lilitangazwa kuwa ni ranchi ya taifa.
Alisema serikali itasimamia mkakati wa kuwagawia maeneo ili waendelee na shughuli zao za kimaendeleo.
Pia Kikwete alisema kuwa atajenga uwanja wa ndege katika eneo hilo ili kurahisisha mawasiliano na usafiri na kwamba, mpango huo utaenda sambamba na kupanua uwanja wa ndege wa Bukoba mjini ili uweze kupokea ndege kubwa.
Kikwete pia aliwaahidi wakazi wa kijiji cha Mtukula mkoani Kagera kwamba, atawaunganishia umeme kutoa nchi jirani ya Uganda na kwamba ameishazungumza na Rais wa nchi hiyo, Yoweri Mseveni.
Alisema wakazi wa mkoa huo wa Kagera watafurahia usafiri wa meli kubwa itakayowaunganisha na wenzao wa mkoa wa Mwanza kupitia ziwa Viktoria.
Alisema meli hiyo itakuwa kubwa kuliko Meli ya MV Bukoba iliyozama mwaka 1996 na kuua watu zaidi ya 900.
Akiwa Kasulu, mkoani Kigoma, Kikwete alitoa ahadi ya kupeleka umeme wilayani humo na kwamba, ahadi hiyo itakwenda sambamba na kuwaletea nishati hiyo wakazi wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Rukwa na Kagera.
Kukithiri kwa vitendo vya wizi na uporaji katika ziwa Viktoria vilionekana kumkera mgombea huyo na kuwahakikishia wakazi wa mikoa hiyo kwamba tayari serikali yake imeanza kuvishughulikia.
Rais Kikwete alisema kuna vikosi vya askari vilivyopelekwa Marekani kupatiwa mafunzo na miezi michache ijayo vitarejea na kupelekwa kwenye ziwa hilo pamoja na vifaa ili kukabiliana na wahalifu hao.
Kwa upande wa wajasiriamali wadogo, Rais Kikwete alisema tatizo lao kubwa ni upatikanaji wa mikopo hivyo, akichaguliwa ataangalia uwezekano wa kuanzisha benki ndogondogo za kuwasaidia.
Aliviahidi kuvipatia mabilioni ya fedha vyama vya ushirika kikiwemo cha Mkoa wa Mwanza (NCU),ili kuvinusuru, lakini akaonya juu ya ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi vyama hivyo.
Pamoja na serikali kuendelea kuvisaidia, aliagiza kuwa ufanyike ukaguzi wa mara kwa mara  ili kuwabana viongozi wabadhilifu kwenye vyama hivyo vya ushirika.
Wakati mgombea urais huyo wa CCM akitoa ahadi hizo, vyama vya Chadema na CUF vilivyoanza kampeni zake mwishoni mwa wiki, navyo vimetoa ahadi zao.
Dk Willibrod Slaa wa Chadema ambaye chama chake kilizizindua kampeni yake jana, alisema watashughulikia mambo makuu tisa wakipewa ridhaa ya kuongoza nchi ikiwemo kufanya mabadiliko makubwa ya katiba na kuifufua Tanganyika ili ikae mezani na Zanzibar kuzungumzia suala la Muungano.
Katika kampeni zake juzi, Profesa Lipumba wa CUF amezungumzia mambo mawili; elimu bure kuanzia shule ya msingii hadi chuo kikuu na kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri ili kubana matumizi ya serikali.

Ahadiza wagombea urais
Jakaya Kikwete
1. Kulinda amani nchini kwa kuzuia chokochoko za kidini, kikabila na kisiasa.
2. Wananchi kutoondolewa kwenye ranchi ya Misenyi
3. Kujenga Uwanja wa Ndege Misenyi
4. Kupanua Uwanja wa Ndege Bukoba
5. Kujenga uwanja wa ndege mkubwa Kigoma
6. Mtukula kupatiwa umeme kutoka Uganda
7. Mikoa ya Kagera, Kigoma, Lindi, Rukwa na Ruvuma kuunganishwa katika gridi ya taifa
8. Kuimarisha Takukuru kwa miaka mitatu
9. Hukumu kwa waliopatikana na hati ya kuua albino
10. Kununua meli kubwa kuliko MV Bukoba
11. Kuanzisha benki ndogondogo kwa ajili ya wajasiriamali.
12. Serikali kulisaidia vyama vya ushirika.
13. Kuimarisha usalama Ziwa Victoria kwa kupeleka kikosi maalum chenye vifaa kupambana na wahalifu
14. Wilya ya Geita kuwa hadhi ya mkoa Januari mwakani.
15. Kulinda muungano kwa nguvu zote.

Profesa Lipumba
1.Elimu ya bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu
2.Kubana matumizi kwa kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri.


Ahadi za Dk Slaa
1.Kujenga nchi isiyo na ufisadi.
2.KufufuaTanganyika ili irejee mezani kujadili muungano na Zanzibar.
3.kufufua uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali zilizopo

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
  • Kupiga Kura

  • Jumapili


Ajali ya Meli ZnZ inatufundisha nini?