|
UBUNIFU wa watafiti nchini Nigeria unaweza kuwa tiba ya ugonjwa mbaya wa ndizi ujulikanao kama Banana Xanthomonas Wilt (BXW) ambao tayari umeshababisha hasara ya dola milioni 500 za Marekani kila mwaka kwa mazao katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ugonjwa huo husababisha ndizi kuvimbavimba kama upele na wakati mwingine ndani kuoza na kukosa radha au kushindwa kuliwa. Agosti 4, mwaka huu, Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA) yenye makao yake nchini Nigeria ilitangaza kupata mafanikio katika kusaka dawa ya ndizi barani Afrika kutoka kwenye pilipili ya kijani.
Utafiti huo umebaini kuwa pilipili ya kijani ina dawa aina ya ferredoxin-kama ilivyo kwa protini ya amphipathic (Pflp) au protini ijulikanayo kama hypersensitive response-assisting protein (Hrap) ambayo inaonekana kuwa protini ambayo inapatia mazao yakiwemo ndizi uwezo wa kuvumilia magonjwa mabaya. "Hrap na Pflp zinafanya kazi kwa kuua kwa kasi kubwa seli ambazo zinagusana na bakteria wanaoeneza ugonjwa," anasema Dk Leena Tripathi, mtaalam wa teknolojia ya mimea katika IITA. Aidha Shirika jingine liitwalo Friends of the Earth Nigeria linasema sasa Afrika imekuwa maarufu kwa kufanyiwa majaribio ya teknolojia ya kisasa ya mimea kwa kulenga katika kile kinachojulikana kama mazao ya watu maskini. "Kitu ambacho Afrika inahitaji kwa sasa ni msimamo wa kiuamuzi kuendeleza mbegu za jadi ikiwa ni pamoja na mchangamano wa kitamaduni na kulinda mazao ya chakula," anasema Mariann Bassey kutoka Friends of the Earth Nigeria.
Kwa upande wake Mratibu wa shirika la Food Sovereignty and Agrofuels Programme, Bassey, ana imani kuwa teknolojia ya mimea itasaidia kuondoa tatizo la njaa ambalo limekuwa likizikumba nchi nyingi za Afrika kila mwaka. Katika ziara yake ya hivi karibuni Uganda, Bassey anasema mkulima mmoja nchini humo alimweleza kuwa walizalisha ndizi kwa kiwango kikubwa lakini ghafla zikaanza kushambuliwa na ugonjwa huo. "Kilimo cha kiikolojia kimemlisha mwanadamu kwa maelfu ya miaka na maboresho yamefikiwa kwa kutumia mbegu vizuri kwa kuzingatia utamaduni, jamii, moyo na mazingira ya hali ya hewa," Bassey aliiambia shirika la habari la IPS.
Lakini Triphathi, mwandishi mkuu wa mada katika utafiki uliochapishwa mwaka 2010 katika jarida la Molecular Plant Pathology, anasema ugunduzi huu ni hatua muhimu katika kupambana na ugonjwa mbaya wa ndizi.
Utafiti unaweza kuwa ni mojawapo ya mafanikio makubwa dhidi ya BXW. Wanasayansi wanasema, ugonjwa wa BXW unaweza kuangamiza uzalishaji wa ndizi na kutishia usalama wa chakula katika maeneo ambapo ni zao kuu la chakula na ambalo linaingiza fedha za kigeni.
Friends of the Earth Nigeria wanasema matumizi ya mbegu mbalimbali na kilimo endelevu ni jambo la msingi katika kufikia mahitaji ya chakula duniani. Shirika hilo linasema ni jambo la msingi kwa wakulima kujihadhari sana na aina mbalimbali za dawa za kisasa. Utafiti wa kisayansi umegundua kuwa hasara ya jumla ya ndizi kutokana na kuambukizwa BXW inafikia kati ya 30 na 52 asilimia, ikiwa na maana kupungua kwa kiasi kikubwa kiasi cha ndizi katika ngazi ya kaya.
Ugonjwa huo, ambao kwanza ulijulikana miaka 40 iliyopita, umeenea katika maeneo yanayolima ndizi kwa wingi kama vile Uganda, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Tanzania. Dalili za ugonjwa ni pamoja na kunyauka majani na kuwa ya njano, huku mmea ukiwa na utando wa njano wa kibakteria, kuiva kwa mkungu wa ndizi kabla ya wakati na kuoza kwa tunda.
Watafiti kutoka IITA, kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Utafiti wa Kilimo na Mfuko wa Teknolojia ya Kilimo Afrika, sasa wako tayari kutathmini maeneo haya yanayokinzana chini ya majaribio ya ndani baada ya Kamati ya Usalama wa Teknolojia ya Mimea Uganda kupitisha majaribio hayo hivi karibuni.
Kulingana na IITA, kwa sasa hakuna kemikali za kibiashara,dawa ya kuzuia kibaolojia au aina ya ndizi inayoweza kustahimili kuenea kwa BXW. Kwa sasa, kuondoa migomba ya kiume miongoni mwa migomba kumeonyesha kuwa na ufanisi kwani ugonjwa huo umeonekana kuambukiza zaidi maeneo yenye migomba ya kiume.Lakini kung’oa migomba hiyo kunahitaji wafanyakazi wengi na baadhi ya wakulima hawana uwezo huo.
Tripathi alisisitiza kuwa hata kama chanzo cha kustahimili ugonjwa kingepatikana, kubuni aina ya ndizi ambayo inastahimili kikweli kweli ugonjwa ni vigumu mno hasa kutokana na asili ya utasa na kukua kwa muda mrefu kwa zao hilo.
Jukwaa la Utafiti wa Kilimo Afrika (FARA) limeweka kipaumbele kwenye jukumu la utafiti katika kukuza uzalishaji wa kilimo. Mkurugenzi mtendaji wa FARA,Dk. Monty Jones, aliwaambia washiriki katika wiki ya 5 ya Sayansi ya Kilimo Afrika iliyofanyika Burkina Faso Julai 2010 kuwa hakuna maendeleo ya kilimo bila utafiti wa kisayansi Afrika.
"Nina imani kuwa utafiti unaweza kufanya mambo makuu katika kilimo barani," anasema Jones. Mwisho
|