
| Mkataba wa wanawake Afrika uwe sheria nchini | Send to a friend |
| Thursday, 02 September 2010 14:04 |
|
SOTE, tunafahamu wanawake wa Afrika ndio wanaoteseka zaidi na majanga mbalimbali kama vita, hali ya ukimbizi na matendo yenye madhara yanayotokana na ukatili wa kijinsia. Kwa kulitambua hilo, Umoja wa Afrika ukaamua kutoa mamlaka kwa Tume ya Afrika ya haki za Binadamu kuandaa Mkataba maalumu wa Haki za wanawake, katika kikao chake cha 31, kilichofanyika Juni 1995, Adis Ababa, Ethiopia. Dhima ya kikao hicho, ni nyongeza kwa Mkataba wa haki za Binadamu wa Afrika wa mwaka 1981. Mkataba huo maalum, ulibainika kuwa haki za wanawake hazikuanishwa kwa upana na, ili kuhakikisha zinazingatiwa, Kituo cha sheria na haki za Binadamu (LHRC) kimezindua tafsiri ya kitabu cha Kiswahili cha nyongeza wa haki za wanawake Afrika (Maputo protocol). Lengo la kuzindua tafsiri hiyo, ni kuhakikisha haki za wanawake wa Afrika, zinazingatiwa na kupewa kipaumbele. “Hadi sasa nchi 46 za Afrika zimesaini, na nchi 27 tayari zimesharidhia Mkataba huo, ikiwemo Tanzania ambayo ilisaini Mkataba huo Novemba 5, 2003 na kuridhia Machi 3, 2007”, anasema Mwaffisi. Kaimu mkurugenzi wa kituo hicho, Imelda Hurio anasema, Mkataba huo endapo utatumika kama sheria ya nchi, utasaidia mambo mengi, ikiwemo kurekebisha sheria ambazo zinaonekana kuwakandamiza wanawake nchini. Haki hizo ni pamoja na kuondoa ubaguzi dhidi ya wanawake, na kwamba nchi wanachama zitaendelea kuingiza katika Katiba za nchi na sheria nyinginezo, ili kuweza kutoa usawa kati ya wanawake na wanaume na kuhakikisha zinatimizwa. Pia, zitaendelea kufuata mtazamo wa jinsia katika maamuzi ya sera, sheria, mipango ya maendeleo na shughuli zote katika upana wa maisha, pamoja na kusaidia harakati za kuondoa ubaguzi Kimataifa, kikanda na kitaifa. Anasema pia mkataba huo utasaidia kuwalinda wanawake wanaoomba hifadhi, wakimbizi, wanaorudi nchini mwao na wale waliohamishwa katika makazi yao, na kwamba nchi wanachama zitachukua hatua mathubuti kuhakikisha hakuna mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 anashiriki katika mapigano au anaajiriwa kama mwanajeshi. Mkataba huo, pia utasaidia kuondoa haki ya kurithi wajane na kupewa haki sawa katika urithi wa madai ya mume wake. Ambapo Mjane huyo atakuwa na haki ya kuendelea kuishi katika nyumba ya ndoa, ikitokea akaolewa tena ataendelea kuwa na haki hiyo hata kama ameondoka. Mkataba huo, utamsaidia mwanamke, kujua haki ya kushiriki katika uchumi wa kijamii, kwa kutambua na kutimiza haki za wanawake wanaopata mshahara mdogo kuwa na posho na stahili sawa na vile wanazopatiwa wanaume wenye mshahara kwa wenzi wao wa ndoa na watoto. Kwa upande wake, Tabu Juma ambaye ni mmoja kati ya wadau wanaopinga unyanyasaji dhidi ya wanawake, anasema mkataba huo utakuwa ni changamoto kwa Taifa zima, kwasababu utamsaidia mwanamke kuweza kutambua haki zake za msingi. “Wanawake wengi, tumekuwa hatujui haki zetu za msingi na badala yake tunaona ni vyema kuendelea kunyanyasika, wakati uwezo na nguvu tunayo”, alisema Tabu. Anasema, anaipongeza serikali kwa kuamua kusaini na kuridhia mkataba huo, ambao utakuwa chachu ya kuletea mabadiliko katika harakati, za kumkomboa mwanamke wa Kiafrika. Kupitia Mkataba huo, ambao serikali hivi sasa inajaribu kurekebisha baadhi ya vipengele ambavyo vinaonekana kumkandamiza mwanamke, ni vyema ipitishe Mkataba huo utumike kama sheria ya nchi. Miongoni mwa wanawake walioshiriki katika uzinduzi huo ni, mtetezi wa haki za wanawake, Salma Mwinyiheri ambaye alifafanua kuwa wanaharakati wa haki za binadamu, wanapaswa kupongezwa kwa jitihada zao za kutoa tafsiri ya mkataba huo, ambao anaamini utasaidia jamii kusoma na kuuelewa kisha kuufanyia kazi. “Kujitolea kwa wanaharakati hao, kupigania haki za wanawake, kumeweza kusaidia hata serikali yetu kuweza kuridhia Mkataba huo”, anasema Mwinyiheri na kuongeza kuwa. Kwa kupitia Mkataba huo wa nyongeza wa haki za wanawake Afrika, utasaidia kuishawishi, Serikali kuufanya uweze kutumika kama sheria ya nchi, itakuwa muhimu kwa wanawake kutambua haki zao. |
| Last Updated on Thursday, 02 September 2010 14:05 |













