MwanzoContactsEmail
Home Habari Mahakamani Ubunge Vunjo ngoma nzito
BOOKMARK THIS PAGE
Ubunge Vunjo ngoma nzito  Send to a friend
Thursday, 02 September 2010 22:18

Daniel Mjema,Moshi
 
KUANGUSHWA katika kura za maoni kwa Mbunge wa zamani wa Vunjo, Aloyce Kimaro kumeibua mambo mazito huku mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro,Vicky Swai akituhumiwa kusuka njama za kuangushwa kwa Kimaro.
 
Wakati hali ya kisiasa ikiwa tete katika Jimbo hilo, Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), naye aliibuka jana akimtuhumu Swai kuwa ndiye aliyesuka mipango ya kumuangusha Kimaro kutokana na maslahi binafsi.
 
Mrema alikuwa akizungumzia uvumi kuwa Kimaro amejiunga na TLP ambapo alikanusha na kusema anachohitaji ni kiongozi bora bila kujali anatoka chama gani na kwamba CCM imefanya makosa makubwa kumuangusha.
 
“Kimaro amefanya mambo makubwa Vunjo kwa kushirikiana na Rais Kikwete ,ameleta Vicoba (benki Vijijini),miradi ya maji, ujenzi wa hospitali ya wilaya na barabara ya Marangu-Kirua itajengwa na ni nguvu zake”alisema Mrema.
 
Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa TLP, alisema ataendeleza yale yote yaliyoanzishwa Kimaro na kusema utakuwa ni ulimbukeni kubeza miradi mikubwa aliyoianzisha ingawa amekuwa mhanga wa hujuma ndani ya CCM.
 
Hata hivyo Swai alipoulizwa jana kuhusu madai hayo mazito dhidi yake, hakukanusha wala kukubali zaidi ya kuhoji inakuwaje Mrema awe msemaji wa Kimaro na kwamba hilo linadhihirisha wapo pamoja kisiasa.
 
“Ninafahamu mpaka tarehe ambayo Mrema na Kimaro walikutana na nipo tayari kuitoa nikirudi huko Moshi sasa hivi niko Dar es Salaam ,Mrema atakuwaje msemaji wa Kimaro kama hawajakubaliana hilo?,”alihoji Swai.
 
Kimaro alipoulizwa alisema matamshi ya Swai katika uzinduzi wa kampeni Jimbo la Vunjo yanadhihirisha kuwa alishiriki katika njama za kumuangusha, lakini akatahadharisha kuwa alichokifanya si kumuangusha yeye bali CCM.
 
“Ni kweli yeye(Swai) ndiye aliyepanga njama za kuniangusha, wewe mwenyekiti wa CCM asiyemsemea mbunge wake ni wa wapi kwa sababu hajawahi kutangaza mafanikio ya CCM Jimbo la Vunjo kwenye mikutano ya hadhara,”alisema.
 
Kimaro alisema mafanikio ya kisiasa ya Mkoa  wa Kilimanjaro yatapatikana tu kama Swai na viongozi wa aina yake watang’olewa huku akisisitiza mwenyekiti huyo hatakwepa lawama kwa yatakayotokea Vunjo na Moshi mjini.
 
“Lakini nawataka wanaonifuatafuata baada ya kura za maoni wasome Mithali 18:18 inayosema ‘kura hukomesha mashindano’ kwa hiyo mashindano ya kura za maoni yaliisha sasa nafanya shughuli zangu”alisisitiza Kimaro.
 
Hata hivyo mshindi wa kura hizo za maoni ambaye ameteuliwa na CCM kupeperusha bendera yake ya Ubunge, Chrispin Meela alisema Kimaro anaogopa kivuli chake na kwamba mlango alioingilia ndio aliotokea.
 
Katika Jimbo la Vunjo, wanachama waliokuwa wakimuunga mkono Kimaro wamehamishia nguvu zao kwa Mrema huku Moshi Mjini wanachama waliokuwa wakimuunga mkono, Athman Ramole wamehamishia nguvu zao Chadema.
 
Jimbo la Moshi linaweza kuwa moja ya majimbo matatu ambayo CCM inaweza kupoteza ushindi kutokana na uhasama na chuki zilizotokana na matokeo ya kura za maoni ambayo yanadaiwa kuwabeba baadhi ya wagombea.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
  • Kupiga Kura

  • Jumapili


Ajali ya Meli ZnZ inatufundisha nini?