MwanzoContactsEmail
Home Habari Habari za Kitaifa Ufisadi wanukia ujenzi ofisi ya RC Dodoma
BOOKMARK THIS PAGE
Ufisadi wanukia ujenzi ofisi ya RC Dodoma  Send to a friend
Thursday, 02 September 2010 22:33

Ramadhan Semtawa
MRADI wa ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma unaonekana kunukia harufu ya rushwa baada ya kuelezwa kuwa utagharimu Sh15 bilioni badala ya Sh2.3 bilioni zilizopitishwa kwa mshindi wa zabuni ya ujenzi wa majengo hayo.

Juzi vyombo vya habari vilimkariri mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk James Msekela akisema mradi huo utagharimu Sh15 bilioni, lakini nyaraka zinaonyesha kuwa mzabuni alishinda kujenga jengo hilo kwa gharama ya Sh2,665,468,680 tu.

Kiwango cha Sh15 bilioni kinaweza kujenga nyumba 12 za ghorofa moja, bwawa la kugolea na huduma nyingine za kifahari kama kila jengo litagharimu kiasi cha Sh1.25 bilioni zilizotumika kujenga nyumba ya gavana wa Benki Kuu (BoT) na naibu wake.

Kauli hiyo ya Dk Msekela imeonyesha kuwa gharama za ujenzi wa jengo hilo zimeongezeka kinyemela kwa takriban mara saba.

Nyaraka ambazo gazeti hili imefanikiwa kuziona zinaeleza kuwa mkandarasi huyo ambaye ni kampuni ya China Railway Jian Chang Eng. Ltd, alishinda zabuni ya kujenga jengo hilo baada ya kuzishindanisha kampuni 12.

Kampuni hiyo pia ina mradi wa ujenzi wa Chuo Kikuu Dodoma

Habari zimeeleza kuwa zabuni hiyo iliyotangazwa na katibu tawala wa Mkoa wa Dodoma (RAS) Aprili 2009, ilifunguliwa Mei 13 mwaka 2009.

Kwa mujibu wa habari hizo kampuni nyingine zilizoshiriki mchakato huo ni Advent Constructon ambayo iliweka dau la kujenga ofisi hizo kwa Sh2.7 bilioni, Dp Sharpriya (Sh2.18bilioni), Stefnat Engineering (Sh 2.15 bilioni), Catic international (Sh 2.12 bilioni).

Kampuni nyingine ni Italframe (Sh 2.11 bilioni), Dh Ladwa (Sh2 bilioni), United Builders (Sh1.95 bilioni), Tanzania Building Works (Sh1.94 bilioni), Masasi Construction (Sh1.78 bilioni), National Service (Sh1.75 bilioni) na Holtan Builders (Sh 1.59 bilioni).  

Kabla hata ya Dk Msekela hajaeleza kuwa mradi huo sasa utagharimu Sh15 bilioni, tayari malalamiko yalianza kujitokeza kupinga uteuzi wa kampuni ya China Railway na kuziacha kampuni zenye tozo dogo.

Malalamiko kuhusu uteuzi wa China Railway yalifikishwa kwa katibu mkuu wa Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA) Januari 8 mwaka huu na akaahidi kuyafanyia kazi.

"Tunathamini mchango wako wa kutafuta ukweli kuhusu jambo hilo na niahidi kwamba tutalifuatilia," alisema Dk R.Mlinga ambaye ni katibu mkuu wa PPRA Januari 25 mwaka huu alipokuwa akijibu malalamiko hayo.

Awali mlalamikaji ambaye si mmoja wa wamiliki walioomba kupewa zabuni hiyo (jina tunalo), aliitaka PPRA kueleza utaratibu uliotumika kumpata mzabuni huyo ambaye gharama zake ni kubwa ikilinganishwa na wengine.

"Hata kama sisi si miongoni mwa watu walioomba zabuni katika mradi huo, kama wanajamii, walipakodi na wadau katika sekta ya ujenzi, tungependa kujua aina ya tathmini iliyotumika kumpata mzabuni huyo," alisema mlalamikaji huyo.

Alipoulizwa kuhusu mchakato huo, Dk Msekela alisema ujenzi ulikwishaanza eneo la Makulu njia ya kuelekea Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na sasa unaendelea.Kwa mujibu wa Dk Msekela, katika mwaka huu wa fedha serikali imetenga Sh3.9 bilioni kwa ajili ya mradi huo.

Alipotakiwa kueleza imekuaje mradi huo sasa ugharimu Sh15 bilioni badala ya Sh2.3 bilioni, Dk Msekela alisema: "Nilisema kama ningepewa kiasi hicho chote cha Sh15 bilioni kwa wakati mmoja, ndiyo jengo hilo lingekamilika katika kipindi cha mwaka mmoja."

Hata hivyo, mkataba ulioingiwa awali na mkandarasi huyo wa Kichina, umeitaka kampuni hiyo kumaliza ujenzi huo kwa gharama ya Sh 2.3 bilioni ndani ya majuma 24.

Alifafanua kwamba jengo hilo ni kubwa na la kisasa na lenye huduma mbalimbali muhimu, ikiwemo kumbi za mikutano na kuongeza, umuhimu wake kwa sasa ni mkubwa.

Dk Msekela, ambaye mwanzoni alizungumza vizuri na mwandishi kwa lugha ya amani, ghafla aligeuka mbogo kadri alivyotakiwa kutoa ufafanuzi wa mchakato wa zabuni, ulioonyesha ongezeko hilo la gharama za mradi.

"Wakati mwingine waandishi mnakuwa na mambo ya kipuuzi sana. Yaani hamuamini wenzenu katika kazi. Sisi jengo limeungua... hapa tunaumiza vichwa ninyi mnafikiri tunakula rushwa hapa," aling'aka.

"Kuweni wazalendo bwana. Hizo nyaraka zako unazoniambia mimi sizijui kama unataka njoo nazo ofisini. Mimi siwezi kuzungumzia kitu ambacho sikijui, njoo ofisini unionyeshe.

"Unasikia, ukiendelea kuniuliza maswali yako hayo nitakata simu, sawa? Yaani hapa kuna watu wengi wanataka huduma,  jengo limeungua wewe unaniuliza maswali ya rushwa. Kwanini hamtaki kuamini wenzenu waliopo madarakani, au wewe umetumwa kuchonokonoa vitu vya hovyo?"  
Mkuu huyo alikiri kuitambua kampuni ya China Railway

lakini kuhusu mchakato huo wa zabuni uliotangazwa na ofisi ya katibu tawala mwaka 2009, alisema: "Zungumza jingine, ukirudia swali lako hili nakata simu."

Dk Msekela alisisitiza kuwa asingependa tena kuulizwa swali kuhusu ufisadi kwani linamkera.
Tuhuma za gharama kubwa za ujenzi wa majengo ambazo zinatiliwa shaka na thamani ya mali,

iliwahi kutikisa ujenzi wa nyumba ya gavana wa BoT na naibu wake ambazo jumla ilikuwa ni sh 3.2 bilioni na baada ya ukaguzi ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilibaini kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni za manunuzi ya umma.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
Last Updated on Friday, 03 September 2010 09:42
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
  • Kupiga Kura

  • Jumapili


Ajali ya Meli ZnZ inatufundisha nini?