|
Kortini kwa tuhuma za uvuvi haramu |
Send to a friend |
|
Thursday, 02 September 2010 22:00 |
|
Burhani Yakub,Tanga
MVUVI mmoja anayeendesha shughuli katika bahari ya hindi Jijini Tanga, Hassan Hussein (25) juzi alifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Mkoa wa Tanga na kutakiwa kujibu mashitaka ya kujihusisha na uvuvi haramu. Ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka wa Serikali, Jenipher Kaaya kwamba mshtakiwa amekuwa na tabia ya kuvua samaki baharini kwa njia ya uvuvi haramu na bila leseni.
Mwendesha mashtaka huyo akishirikiana na Innocent Mhina alidai kuwa August 26 mwaka huu saa 11.15 jioni huko katika eneo la Mto Utofu, mshtakiwa huyo alikamatwa na ofisa wa idara ya uvuvi ya Jiji la Tanga Hyacinth Wariro akiwa na aina mbili za samaki waliovuliwa kwa njia ya haramu.
Alidai kuwa ofisa huyo na wenzake wakiwa katika doria ya kupambana na wavuvi haramu walipochunguza walibaini kuwa samaki hao hawakuvuliwa kwa njia za halali.
Waendesha mashtaka hao walidai mtuhumiwa huyo pia alipotakiwa kuonyesha leseni yenye kumruhusu kuvua katika bahari ya hindi hakuweza kuonyesha. Kwa mujibu wa maelezo ya waendesha mashtaka hao wakati wakisoma mashtaka hayo ni kuwa mshtakiwa alikamatwa akiwa na samaki aina ya Changu na Tembo wote wakiwa na uzani wa kilo 20.
Mshitakiwa alikana mashtaka hayo yote mawili na yuko nje kwa dhamana hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Septemba 29 mwaka huu.
|