|
Wakamata zana haramu za uvuvi |
Send to a friend |
|
Saturday, 28 January 2012 08:53 |
|
Lilian Lugakingira, Bukoba KIKOSI cha Ulinzi wa Raslimali za Ziwa Victoria Kanda ya Kagera, kimekamata nyavu za uvuvi haramu 250 zenye thamani Sh2 milioni na mitumbwi 11 inayotumia kasia.
Zana hizo haramu zilikamatwa kwenye mwalo wa Kyandiba, ulioko Bukoba vijijini mkoani Kagera, zilikuwa zikitumika kwa shughuli za uvuvi kinyume cha sheria, ikiwamo mitumbwi ambayo haina usajili. Akizungumzia operesheni hiyo iliyofanyika ghafla jana, Ofisa mfawidhi wa kikosi hicho, Rodrick Mahimbali, alisema nyavu zenye matundu madogo chini ya inchi sita, haziruhusiwi kutumika kwa shughuli za uvuvi, maana zinakamata samaki wachanga na kuharibu mazalia yao.
Mahimbali alisema kwenye oparesheni hiyo, samaki wachanga wabichi aina ya sangara takriban kilo 900 walikamatwa wakiwa katika harakati za kusafirishwa kupelekwa sokoni.Aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri ambazo zitafanikisha kukamakwa kwa wavuvi haramu na kuwezesha kuwapo uvuvi endelevu.
Baadhi ya wavuvi waliokuwa katika mwalo huo, walishukuru kikosi hicho na kukiomba kuongeza nguvu kukabiliana na vitendo vya uvuvi haramu, ambavyo vinasababisha wananchi kuendelea kuwa maskini.
Walisema uvuvi haramu unasababisha kukosekana kwa samaki, hasa kwa wavuvi wanaotumia nyavu zenye matundu makubwa.“Tunaomba wanaokamatwa wafilisiwe, badala ya kuwalipisha faini na kurejeshewa mali zao,” alisema mmoja wavuvi hao.
|